Ufunuo Mtakatifu

Mafundisho ya Waanzilishi wa dini za dunia wamehuisha mafanikio makubwa katika fasihi, usanifu majengo, sanaa na muziki. Wameendeleza uwezo wa kufikiri, sayansi na elimu. Kanuni zao za kimaadili zimetafsiriwa kama sheria kwa watu wote, zikiongoza na kuinua mahusiano ya watu. Watu hawa waliowezeshwa kwa uwiano sawa sawa huitwa Wadhihirishaji wa Mungu katika maandiko ya Kibaha’i, na hujumuisha (kati ya wengine wengi) Krishna, Musa, Zoroaster, Buddha, Yesu Kristo, Muhammad, Bab na Baha’u’llah. Historia hutoa mifano isiyo na idadi ya Watu hawa ambao huamsha ndani ya umati wa watu uwezo wa kupenda, kusamehe, kujali, kuthubutu kwa kiwango kikubwa, kuondokana na chuki, kujitoa dhabihu ili kuboresha hali nzuri ya wote, na kudhibiti tabia zisizofaa za binadamu. Mafanikio haya yanaweza kufahamika kama urithi wa pamoja wa kiroho wa jamii ya binadamu.

Imani ya Kibahá’í ilianza na dhima iliyokabidhiwa na Mungu kwa Wadhihirishaji Watakatifu wawili—Báb na Bahá’u’lláh.

Akizaliwa karne mbili zilizopita, mnamo Oktoba 1819, Báb alitangaza kwamba Yeye alikuwa mchukuzi wa ujumbe uliokusudiwa kubadilisha maisha ya wanadamu, ambayo yalikuwa yamefikia kwenye ukingo wa zama mpya. Aliitisha marekebisho ya kiroho na kimaadili, kuboresha nafasi ya wanawake na hatima ya masikini. Alianzisha dini tofauti na inayojitegemea, akiwahamasisha wafuasi Wake kubadilisha maisha yao na kutekeleza vitendo vikubwa vya ushujaa. Dhima ya Báb ilikuwa ni kuandaa njia kwa ajili ya Bahá’u’lláh.

Baha’u’llah—kama wa mwisho katika mtiririko wa waelimishaji waliouhishwa kiroho ambao huongoza jamii ya binadamu kutoka kipindi kimoja hadi kingine—ametangaza kuwa jamii ya binadamu inaelekea kipindi kilichokuwa kikingojewa kwa muda mrefu cha ukomavu: umoja katika ngazi ya ulimwengu wa asasi za kijamii. Anatoa mtazamo wa umoja wa jamii ya binadamu, mfumo wa kimaadili, na mafundisho ambayo, yakiwa na msingi unaokubali upatano wa sayansi na dini, hushughulikia matatizo ya kipindi hiki moja kwa moja. Huongoza njia kwa ajili ya hatua inayofuata ya muendelezo wa hali ya kijamii ya watu. Huwapatia watu wa jamii ya dunia hadithi inayounganisha inayoendana na uelewa wetu wa kisayansi wa uhalisia. Hutuita kutambua ubinadamu wetu mmoja, kujiona kama watu wa familia moja, kuondokana na uadui na chuki, na kuungana pamoja. Kwa kufanya hivyo, watu wote na kila kundi la kijamii linaweza kuwa wasukumaji wa kubumba siku zao zijazo, na, mwishowe, ustaarabu wa dunia wenye haki na amani.

Filamu fupi: Mawazo juu ya dini moja inayoendelea kufunguka na ukomavu wa jamii ya binadamu

Mjumuiko wa Maandiko ya Baha’u’llah na Báb huonwa na Wabahá’í kuwa Ufunuo kutoka kwa Mungu. Hufanya msingi wa Imani ya Kibaha’i. Kwa kipindi chote cha miaka mingi ya kifungo Chake, Baha’u’llah alifunua vifungu vingi, vikiwa sawa na zaidi ya vitabu100. Hapa chini ni baadhi ya mateuzi toka bahari hii kubwa.

Mlango wa maarifa wa Aliye Mkale umekuwa na utaendelea kuwa, umefungwa mbele ya macho ya watu. Hakuna mtu mwenye uelewa ambaye atapata kufikia baraza Lake takatifu. Kama ishara ya rehema Yake, hata hivyo, na uthibitisho wa upendo Wake wa ukarimu, Yeye amefunulia watu Nyota Zake za maongozi matakatifu, Ishara za umoja Wake mtakatifu, na ameamuru utambuzi wa Watu hawa walitakaswa kuwa sawa na utambuzi wa Asili Yake mwenyewe.

(Makusanyo toka Maandiko ya Baha’u’llah)

Vioo hivi vilivyotakaswa…ni, kila mmoja na wote, Vielelezi duniani vya Yeye ambaye ni kitovu cha ulimwengu, kiini na Kusudi la mwisho. Kutoka Yeye hutokea maarifa yao na nguvu; kutoka Yeye hupatikana mamlaka yao.

(Kitabu cha Yakini)

Wakiongozwa na nuru isiyoshindwa ya maongozi, na wakijazwa na mamlaka ya juu, Wao hupewa mamlaka kutumia uhuisho wa maneno Yao, matamko ya rehema Zao zisizo na dosari na pepo zihuishazo za Ufunuo Wao kusafisha kila roho inayonuina na roho pokevu kutoka uchafu na vumbi la kujali mambo ya kidunia na yenye mapungufu.

(Makusanyo toka Maandiko ya Baha’u’llah)

Hii ni Imani ya Mungu isiyobadilika, ya milele katika muda uliopita, ya milele kwa siku zijazo.

(Hema la Umoja)

Hii ni Siku ambayo Baraka za juu kabisa za Mungu zimemwagwa juu ya watu wote, Siku ambayo rehema Yake isiyokikomo kabisa imeingizwa ndani ya viumbe vyote. Inawapasa watu wote wa duniani kuondokana na tofauti zao, na kwa umoja na Amani kamili, kuambatana pamoja chini ya Mti wa kujali Kwake na upendo-wa-ukarimu.

(Makusanyo toka Maandiko ya Baha’u’llah)

Kile ambacho Bwana ameamuru kama tiba kamili na chombo cha juu cha uponyeshaji wa jamii nzima ya binadamu ni muunganiko wa watu wote katika Hoja moja ya ulimwengu, Imani moja.

(Muito wa Bwana wa Majeshi)

Ninyi ni matunda ya mti mmoja, na majani ya tawi moja. Tendeaneni mmoja kwa mwingine kwa upendo na upatano wa hali ya juu, kwa urafiki na uelewano. Yeye ambaye ni Nyota ya Ukweli hunishuhudia! Ni wenye nguvu mwanga wa umoja kwamba unaweza kuangazia dunia nzima.

(Waraka kwa Mwana Mbwa-Mwitu)

Dunia ni nchi moja, na binadamu ni raia wake.

(Waraka wa Baha’u’llah, Lawh-i-Maqsud)

Wale ambao wamejaliwa ukweli na uaminifu sharti waambatane na watu wote na jamii zote za duniani kwa furaha na wangavu, kwa kuwa kuambatana na watu kumekuwa na kutaendelea kuwa jinsi ya kuendeleza umoja na upatano, ambavyo pia ni vya muhimu kwa kudumisha utaratibu duniani na ufanyaji upya wa mataifa.

(Nyaraka wa Baha’u’llah, Tarazat)

Funga macho yako toka utepetevu, na kazia mtazamo wako kwenye umoja. Shikilia kwa nguvu kwa kile ambacho kitaongoza kwa hali nzuri na utulivu wa binadamu wote.

(Nyaraka za Baha’u’llah, Kalimat-i-Firdawsiyyih)

Asiwatakie wengine kile ambacho yeye mwenyewe asingejitakia, wala kuahidi kile ambacho hawezi kutimiza.

(Kitabu cha Yakini)

Mfikirie mtu kama chimbo la madini lililojaa vito vya thamani. Elimu pekee, yaweza, kufichua hazina zake na kuwezesha binadamu kunufaika kutoka humo.

(Waraka wa Baha’u’llah, Lawh-i-Maqsud)

Maarifa ni kama mabawa kwa maisha ya mtu, na ngazi kwa mpando wake. Ni ya lazima kwa kila mmoja.

(Nyaraka za Bahá’u’lláh, Tajallíyát )

Uwe mkarimu katika ufanisi na mwenye shukrani katika taabu. Uwe mwenye kustahili uaminifu wa jirani yako na umwangalie kwa uso mwangavu na wa kirafiki. Uwe hazina kwa masikini, mwonyaji kwa tajiri, mwitikaji kwenye mlio wa mhitaji, mhifadhi wa utakatifu wa ahadi yako. Uwe na haki katika hukumu yako na mwangalifu katika maneno yako. Usiwe mwenye dhuluma kwa mtu yeyote, na uonyeshe upole wote kwa watu wote. Uwe kama taa kwa wale ambao hutembea katika giza, furaha kwa mwenye huzuni, bahari kwa mwenye kiu, pepo kwa wenye fadhaa, msaidizi na mtetezi wa yule aliyepatwa na dhuluma. Acha ukamillifu na tabia ya unyofu vitofautishe vitendo vyako vyote. Uwe nyumba kwa mgeni, kitulizo kwa mwenye mateso, tegemeo kuu kwa mkimbia hatari. Uwe macho kwa kipofu, na nuru kwa uongozi kwa miguu ya mpotovu. Uwe pambo kwa uso wa ukweli, taji kwa paj la uso la uamnifu, nguzo ya hekalu la haki, pumzi ya uzima mwili wa wanadamu, safina juu ya bahari ya hekima, jua katika mbingu ya baraka, kito cha thamani kwenye taji la hekima, nuru ing’arayo katika mbingu ya kizazi chako, tunda juu ya mti wa unyenyekevu.

(Waraka kwa Mwana Mbwa-Mwitu)

Kuna Mwondoa Shida yeyote isipokuwa Mungu? Sema: Mungu asifiwe! Yeye ni Mungu! Wote ni watumishi Wake na wote hutii amri Yake!

(Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Jiondolee mwenyewe miambatano na vyote isipokuwa Mungu, jitajirishe mwenyewe katika Mungu kwa kuachana na mengine yote pembeni Yake, na sema sala hii:
Sema: Mungu hutosheleza vitu vyote juu ya vitu vyote, na hakuna chochote mbinguni ama duniani ama katika chochote kilicho kati yao isipokuwa Mungu, Bwana Wako, hutosheleza. Hakika, Yeye mwenyewe ndie Mjuaji, Mtoshelezaji, Mweza yote.

(Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Ee Bwana! Kwako Wewe najileta kwa kimbilio, na kuelekea ishara Zako zote nageuzia moyo wangu. Ee Bwana! Nikiwa safarini au nyumbani, na katika shughuli zangu au katika kazi yangu, naweka Imani yangu yote Kwako.
Nijalie basi msaada Wako utoshelezao ili unifanye kuwa huru kwa vitu vyote, Ewe Ambaye hupitwi na yeyote katika rehema Yako! Nijalie fungu langu, Ee Bwana, kama upendavyo Wewe, na unifanye niridhike na chochote kile ambacho Wewe umeakiamuru kwa ajili yangu.
Yako ni mamlaka halisi kuamuru.

(Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Sala inayokubalika kabisa ni ile ambayo imetolewa katika hali ya juu kabisa ya kiroho na ya furaha; urefushaji wake haujawahi kuwa na sio kipenzi cha Mungu. Sala inapokuwa imejitenga zaidi na safi zaidi, ndivyo inakuwa ya kukubalika zaidi mbele ya uwepo wa Mungu.

(Bayán ya Kiajemi, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Hupendeza kwamba mtumishi lazima, baada ya kila sala, kumsihi Mungu kutoa rehema na msamaha kwa wazazi wake.

(Bayán ya Kiajemi, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Mimi ni Nukta ya Asili ambayo kutokea kwake vimetengenezwa vitu vyote vilivyoumbwa. Mimi ni Sura ya Mungu Ambaye mwangaza Wake haujawahi kufunikwa, Nuru ya Mungu Ambaye unurishaji wake haujawahi kufifishwa.

(Waraka kwa Muhammad Shah, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Kile ambacho Mungu ameniumba nacho Mimi sio udongo ambao wengine wameumbiwa nao. Yeye amenijalia juu Yangu kile ambacho wale wa kidunia hawawezi kuelewa, wala waaminifu kuvumbua.

(Waraka kwa Muhammad Shah, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Ni bora kuongoza roho moja kuliko kumiliki vitu vyote ambavyo vipo duniani, kwani kwa wakati wote ambao roho hii iliyoongozwa ipo chini ya kivuli cha Mti wa Umoja Mtakatifu, yeye na yule ambaye amemuongoza pamoja watakuwa wapokezi wa rehema za upendo wa Mungu, wakati ambapo umiliki wa vitu vya kidunia utakoma wakati wa kifo. Njia ya uongozi ni ile ya upendo na huruma, na sio ya mabavu na mvutano. Hii imekuwa njia ya Mungu kwa siku zilizopita, na hii itaendelea kuwa kwa siku zijazo!

(Bayán ya Kiajemi, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)

Bwana wa ulimwengu hajawahi kamwe kumuinua mtume ama Yeye kushusha Kitabu isipokuwa tu kama Yeye ameweka agano Lake na watu wote, akiwaita wao kwenye upokevu wao wa Ufunuo unaofuata na Kitabu kinachofuata; kwa sababu rehema Zake hazina kikomo na ni bila mipaka.

(Bayán ya Kiajemi, Mateuzi kutoka Maandiko ya Báb)